Uchambuzi wa Migogoro katika Maeneo ya Pwani nchini Kenya na Tanzania

Ripoti hii inatoa taswira ya mienendo ya migogoro katika maeneo muhimu ya Pwani ya Kenya na Tanzania. Taarifa hii imekamilishwa kutokana na mradi wa “Kujenga Amani: Building Peace in the Swahili Coast”, mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na shirikisho la asasi za kiraia (CSOs) likiongozwa na taasisi ya CEFA Onlus. Lengo kuu la mradi huu ni kuona nafasi iliyoimarika kwa mitandao ya vijana na jumuiya za ngazi ya chini katika kuhamasisha vijana wanaoishi katika maeneo ya pwani ya Kenya, Msumbiji na Tanzania ili waweze kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya katika jamii zao. Mradi unatumia dhana ya kuongozwa na jamii ambayo inatambua kwamba jitihada zinazofanywa na taasisi za ngazi ya chini ni muhimu sana katika kufikia amani ya kudumu, na kutambua umuhimu wa kuwawezesha mtu mmoja mmoja, familia na jamii kwa jumla kuwa wadau muhimu katika juhudi za kuimarisha amani.